Thursday, 22 September 2016

TATHMINI YA UREJESHAJI WA ARDHI NA MASHAMBA KWA WANANCHI KUTOKA KWA WAWEKEZAJI NCHINI













Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imedhamiria kutatua tatizo la wawekezaji katika ardhi na mashamba
wasiokuwa na dhamira njema na maendeleo ya nchi hii.Hili limejidhihirisha dhahiri katika zoezi linaloendelea la kubaini maeneo husika na kuyabatilisha kutoka kwa wamiliki husika na kupatiwa wananchi kuyaendeleza sambamba na agizo la Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli.Hivi karibuni, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mheshimiwa William Lukuvi alizitaka halmashauri zote nchini, kufanya uhakiki wa mashamba makubwa ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu na kutoa notisi kwa wamiliki wake ili wafahamu hatua zitakazochukuliwa na Serikali.Alisema hayo wakati akitangaza kwa wananchi wa Tanga kuhusu kufutwa kwa hati miliki ya mashamba matano ya mkonge yaliyopo wilaya za Muheza na Pangani. Mashamba hayo ni Lewa Estate, Kipumbwi, Azimio, Bwembwera na
Sakula.Mheshimiwa Lukuvi alisema; “Mheshimiwa Rais alifikia uamuzihuo Desemba 19, mwaka jana baada ya kujiridhisha kuwa wamiliki wake wameshindwa kuyaendeleza mashamba hayo kwa shughuli zilizokusudiwa kama walivyokuwa wameomba katika vijiji husika”.Mheshimiwa Lukuvi aliuagiza mkoa wa Tanga, upendekeze mali zilizopo kwenye mashamba hayo, kama majengo ya ofisi na mali nyingine
wapewe watu gani kwa ajili ya maendeleo ya eneo husika kabla mashamba hayo hayajagawiwa.
Pia, aliagiza kuwa mkoa lazima uhakikishe wamejua idadi kamili ya wananchi walioko katika mashamba hayo na kiasi cha ardhi iliyopo, ikiwepo kufanya utaratibu pia wa ulipaji wa fidia kwa wale
wanaostahili.Aidha, amani iliyokosekana kwa takriban miaka kumi katika Kijiji cha Kapunga wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya, imerejea baada ya Mheshimiwa Lukuvi kuwatangazia wananchi kurejeshwa kwa hekta 1,870 zilizounganishwa kimakosa kwenye shamba la mwekezaji mwaka 2005. Awali mwaka 1985, Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, aliwaomba wakazi wa Kijiji cha Kapunga eneo lenye ukubwa wa hekta 5,500 ili kupata eneo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, na hasa kuboresha kilimo nchini. Wananchi walikubali ombi hilo la Mwalimu Nyerere na kutoa hekta hizo. Lakini, wananchi hao
wa Kapunga walishangazwa baadaye kuona kuwa hata yale maeneo waliyobaki nayo, yakafanywa kuwa ya mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Export Trading Group, Katika kipindi hicho chote cha miaka kumi,
wananchi wa Kapunga wamekuwa wakipata matatizo ya aina mbalimbali katika eneo hilo, kwa Export Trading Group
kujichukulia maeneo mengine ya wananchi hao. Baadhi ya mateso
waliyopata kutoka kwa mwekezaji huyo ni kuvunjiwa daraja, kumwagiwa sumu katika mashamba yao n.k.
 Hatahivyo baada ya agizo la Rais la kumtaka mwekezaji huyo, kurejesha kiasi cha hekta 1,870wa wananchi, maeneo hayo sasa ni ya wananchi.
Mheshimiwa Lukuvi alitangaza; “Tumekaa na kukubaliana, kiasi hiki cha ardhi kirejeshwe kwenu na mwekezaji amekubali hekta hizo sasa ni mali ya kijiji chenu”.Zoezi limeendelea katika mikoa ya Morogoro na Tanga, ambapo hati za miliki za mashamba makubwa 13 yenye zaidi ya ekari 24,000, yaliyoagizwa na Mheshimiwa Rais Magufuli, zilifutwa na mashamba hayo kukakabidhiwa kwa wananchi wasio na ardhi. Serikali imetakiwa itenge maeneo mengine kwa ajili ya uwekezaji katika mikoa
hiyo, baada ya wamiliki wake kushindwa
kuyaendeleza.Mheshimiwa Lukuvi alisema: “Sheria ya vijiji inaruhusu vijiji kumilikisha ardhi isiyopungua ekari 50 kwa kuitisha mkutano wa kijiji ili uridhie, lakini baadhi ya viongozi wamekuwa wakishirikiana na wawekezaji matapeli ili wapewe ardhi kwa njia za hila”.
Vile vile akiwa wilayani Monduli mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Lukuvi alikabidhi ekari 39,924 za mashamba kwa wananchi, baada ya Mheshimiwa Rais Magufuli kufuta hatimiliki za wawekezaji 13.
Akiongea na wananchi wa kata za Lokisale na Olmoti katika mkutano wa hadhara, Mheshimiwa Lukuvi alisema; “Rais amefikia hatua hiyo baada
ya wawekezaji hao kushindwa kuyaendeleza
mashamba waliyokabidhiwa kwa ajili ya kilimo cha biashara na kuwaacha wananchi bila ardhi”. Kwa ujumla, Wizara ya Ardhi inaendelea
kushughulikia umilikishaji ardhi usiofuata sheria katika maeneo mengi nchini. Mathalani, katika wilaya ya Simanjiro mkoa wa Manyara, wanakijiji wa Kilombero Kata ya Shambarai, wamerudishiwa ekari 828 za mashamba manne yaliyochukuliwa na familia moja baada ya kujimilikisha bila kufuata sheria. Familia ya watu wanne wa kijiji hicho,
walijimilikisha ekari 1,028 bila kufuata kanuni, taratibu na sheria za ardhi, hivyo wananchi hao wakawanyang’anya ekari 828 na kuwaachia ekari
200.Aidha, zaidi ya mashamba 35 yanatarajiwa
kubatilishwa milki na Serikali ndani ya mwaka huu 2016.

Source;: www.ardhi.go.tz

No comments:

Post a Comment